Zantel Yazindua Kifurushi Maalumu kwa Watalii Zanzibar


Zanzibar-Novemba 2017. Zantel kwa mara ya kwanza imeanzisha huduma ya kipekee ya kifurushi kwenye laini zake maalumu za simu ambacho kitakuwa na muda wa maongezi pamoja na data kwa ajili ya watalii kilichopewa jina la 'Tourist Pack'.

Kifurushi hicho kipya kitawawezesha wageni wanaosafiri kwenda Zanzibar, kupiga simu za ndani na nje ya nchi katika nchi sita za Ulaya ambazo ni Uingereza, Uhispania, Denmark, Italia, Ufaransa na Marekani kwa bei nafuu zaidi. 

Akizindua kifurushi hicho maalumu katika hafla ya mkutano na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Mkurugenzi wa Zantel Zanzibar, Mohamed Mussa Baucha alisema kifurushi hicho cha malipo ya kabla ambacho kimewalenga zaidi watalii kitakua na ofa ya dakika za kupiga simu za kimataifa na za  hapa nchini ikiwa ni pamoja na kifurushi cha intaneti ndani ya mwezi mmoja.

Aliongeza kuwa kifurushi hicho maalumu kimelenga kuwasaidia watalii kurahisisha njia ya kuendelea kuwasiliana na ndugu au familia zao pindi wanapotua Zanzibar.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo alisema, Zantel imeamua kuja na kifurushi hicho kwa ajili ya watalii baada ya kufanya utafiti mdogo ambao unaonyesha kwamba watalii wengi huhitaji huduma ya mawasiliano ya simu sambamba na huduma ya mtandao pindi tu wanapofika katika hoteli mbalimbali mjini hapo.

"Wakati watalii wanapofika Zanzibar, mara nyingi jambo la kwanza huwa wanauliza kuhusu upatikanaji wa mtandao, Wi-Fi na intaneti jambo ambalo linadhihirisha mawasiliano ya simu ni jambo la msingi kwao. Hilo limetusukuma kuanzisha huduma hii ili kurahisisha mawasiliano yao, "alisema mkurugenzi huyo wa Zantel-Zanzibar.

Alisema kifurushi hicho kipya kitamzawadia mteja dakika 10 za kupiga Zantel kwenda Zantel, dakika 10 za kupiga zantel kwenda mitandao mingine na dakika 5 kwa simu za kimataifa zikiwamo nchi za Ufaransa, Italia, Denmark na Marekani.

Pia kifurushi hicho kipya kitampa mteja GB 4 kwa ajili ya intaneti kwa mwezi ambapo kitakapokwisha mteja anaweza kuchagua vifurushi vya muda wa maongezi na data kwa ofa zinazotolewa na Zantel.

Aliongeza kwamba kila laini ya simu kwa huduma hii, itauzwa Dola 10 za Marekani au Shilingi ya Kitanzania inayoendana na thamani hiyo ya fedha. Na watumiaji watapaswa kufuata hatua za kujisajili zilizo chini ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Akitoa taarifa nyingine kwenye mkutano huo mjini Zanzibar, alisema Zantel inalipa kodi ya shilingi bilioni 2 Serikalini kwa kila mwezi na kiasi cha Shilingi  bilioni 24  kwa mwaka.

Aliongeza kuwa Sekta ya utalii inachangia kwa asilimia 25 hadi 27 kwenye bajeti yam waka Zanzibar na akasisitiza kuna haja ya kuimarisha zaidi sekta hiyo ya utalii ili kuongeza watalii wengi kutembelea Zanzibar.

Kwa maelezo zaidi, tutumie ujumbe

Angalia Kama Unapata Huduma

Tafuta duka la Zantel