Zantel Yaungana Na Bodi Ya Mapato Zanzibar Kukusanya Kodi


14 Desemba 2017. Zanzibar. Zantel kwa kushirikiana na Bodi ya Mamlaka ya Mapato ya Zanzibar wameingia katika makubaliano ambayo yatawawezesha wakazi wa kisiwani hapa kurahisisha huduma ya ulipaji kodi kwa njia ya simu kupitia huduma ya EzyPesa inayotolewa na Kampuni ya Mawasiliano ya Zantel.

Ushirikiano huo unawezesha wateja wote wa Bodi ya Mapato Zanzibar kuweza kufanya miamala ya malipo ya kodi bila usumbufu wowote kupitia EzyPesa.

Hii inamaanisha kwamba walipa kodi wa ndani wataweza kulipa kodi zao husika ikiwamo ushuru wa forodha na kodi zingine kama PAYE na VAT kwenye uingizaji wa biadhaa kupitia mfumo wa EzyPESA.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini ya makubaliano hayo Alhamisi ya tarehe 14 Desemba 2017, Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Sherif El Barbary akiwa ameambatana na Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Amour Hamil Bakari na Mkuu wa Zantel Zanzibar, Mohamed Mussa (Baucha) alisema lengo kuu la huduma hiyo ni kuwawezesha wakazi wa Zanzibar kulipa kodi kwa urahisi zaidi kupitia huduma ya EzyPesa ya Zantel.

Alisema kuwa hatua hiyo ya makubaliano inaendana sawa na dira ya Bodi ya Mapato Zanzibar, yenye lengo la kuwa kitovu cha ukusanyaji mapato chenye ufanisi, jambo ambalo litaiwezesha  nchi kuongeza pato la taifa la ndani kwa mwaka (GDP).

“Kama tunaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kupitia huduma ya EzyPesa na pato la Taifa GDP litaongezeka zaidi. Hii itasaidia kuimarisha uchimi wa Taifa zima, na kwa namna nyingine kipato cha mwananchi wa kawaida kitaongezeka.

Alisema Zantel ni miongoni mwa kampuni inayoongoza katika kuchangia malipo makubwa ya kodi kwa Serikali ya Zanzibar na mtandao huo utaendelea kuhakikisha unaendelea na utaratibu wa kusaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja  na Bodi ya Mapato ya Zanzibar ili kuhakikisha kwamba  wanakusanya kodi kwa kadri wanavyoweza kupitia huduma ya EzyPesa.

Takwimu zinaonyesha kwamba Zantel inalipa Shilingi bilioni 2 kama kodi kwa serikali ya Zanzibar kila mwezi ambapo ni takribani shilingi 24 bilioni kwa mwaka.

“Lengo la ushirikiano huu ni kuhakikisha tunawasogezea wananchi huduma za ulipaji kodi karibu na maeneo yao, nikimaanisha kuwa sasa hawatohitaji kupoteza muda mwingi kuzifuata huduma za kodi ofisini kwetu bali zitakuwepo viganjani mwao,” alisema Kamishna wa Kodi wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Amour Hamil Bakari.

Alisema lengo kuu la Bodi ya Mapato Zanzibar ni kusogeza huduma karibu kwa wateja wake, kuimarisha shughuli za utendaji wa kila siku za taasisi hyo ikiwa ni pamoja na kubuni mbinu mbadala za kuongeza ukusanyaji wa mapato Zanzibar.

Kwa maelezo zaidi, tutumie ujumbe

 

Angalia Kama Unapata Huduma

Tafuta duka la Zantel