Zantel yatoa milioni 10 kwa Jumuiya ya Wakulima wa Mwani Zanzibar


 Katika jitihada za kukuza ujasiriamali pamoja na kuongeza uwezo wa wanawake katika kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi, kampuni inayoongoza visiwani Zanzibar, Zantel, leo imetoa kiasi cha shillingi millioni 10 kwa Jumuiya ya Wakulima wa mwani Zanzibar.

Kampuni ya Zantel pia itaandaa mafunzo ya ujasiriamali, utawala na usimamizi kwenye maswala ya fedha kwa zaidi ya wanawake 2000 yatakayoendeshwa katika kipindi cha mwaka 2016 na 2017.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Afsa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Zantel, Bwana Benoit Janin alisema msaada wa Zantel kwa Jumuiya ya Wakulima wa mwani Zanzibar unaendelea kuonyesha jitihada za kampuni ya Zantel katika kutekeleza ahadi zake kwa ajili ya ustawi wa jamii ya wanawake.

‘Wanawake wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la upatikanaji wa rasilimali,maarifa na huduma, hivyo basi ili kukabiliana na changamoto hizi tunaamini msaada utabadilisha maisha ya wanawake wengi wanaotegemea mradi huu katika  kuendesha maisha’ alisema Bw.Janin.

Kilimo cha mwani ni shughuli muhimu ya kiuchumi inayotegemewa na wakazi wanaoishi katika miamba ya matumbawe ya visiwa vya Unguja na Pemba. Aina hii ya kilimo inafanywa zaidi na wanawake kwani kati ya wakulima 23,654 asilimia 80% ni wanawake.

'Imani yetu kama Zantel ni kuwa uwezeshaji wa wanawake ni jambo muhimu na sahihi la kufanya, kwa sababu mwanamke ndiye nguzo ya jamii na hivyo tukitoa fursa za kiuchumi kwa wanawake tutaigusa jamii pana zaidi’ alisema Bi Rachel Samren, Mwenyekiti wa Bodi wa Zantel na Makamu wa Rais wa Mambo ya nje wa Millicom.

Akitoa shukurani zake za kwa kampuni ya Zantel, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakulima wa mwani Zanzibar, Bi Pavu Mcha Khamis alisema msaada waliopewa na kampuni ya Zantel utasaidia kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kilimo kama kamba kwa ajili ya kilimo cha mwani.

'Kwa kipindi kirefu tumekuwa tunakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo tunaishukuru kampuni ya Zantel kwa kutusaidia kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kilimo pamoja na fursa za masoko hivyo kuwaongezea wanachama wetu kipato’ alisema Bi Pavu Mcha Khamis.

Jumuiya ya Wakulima wa mwani Zanzibar ilianzishwa mnamo mwaka 2010,kwa lengo la kuwaunganisha wakulima wote wa zao la mwani Zanzibar ili kuwawezesha kupata muongozo wa kukuza na kuendesha kilimo bora cha mwani kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kupanua soko la zao hilo.

Kwa maelezo zaidi, tutumie ujumbe

Angalia Kama Unapata Huduma

Tafuta duka la Zantel