Zantel Yaanza Mradi Mkubwa Kuboresha Mawasiliano


Kampuni ya simu ya Zantel imeanza kazi ya kuboresha mtandao wake na kuwa kisasa ambao utakidhi mahitaji ya mawasiliano kwa wateja wake, baada ya kuwasili kwa vifaa kamili pamoja na mitambo yake yenye thamani ya shilingi bilioni 22 itakayofungwa katika visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya Tanzania Bara kwa kushirikiana na Kampuni za Ericsson na Huawei Technologies.

Kampuni hiyo ya Zantel ambayo kwa sasa ipo chini ya Millicom Group iliyonunua asilimia 85 ya hisa za kampuni hiyo, ilionesha mitambo hiyo ya kisasa mbele ya waandishi wa habari pamoja na wadau wengine wa kampuni hiyo, katika hafla fupi iliyofanyika eneo la Mombasa, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Mkuu wa Kampuni ya Zantel Zanzibar Mohamed Khamis Baucha amesema maboresho hayo yatarahisisha mawasiliano na kuongeza kasi na ubora wa hali ya juu, na kuahidi kuwa kazi hiyo itafanyika kwa muda wa miezi mitatu hadi kukamilika kwake.

"Ni miezi minane tangu Milicom waliponunua hisa Zantel, na lengo kuu ni kuboresha mawasiliano katika visiwa vya Unguja na Pemba" alisema Baucha.

Aliongeza kuwa hivi sasa Zantel inachangia kiasi cha shilingi bilioni 2 kila mwezi inayotokana na kodi na imani yao kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo huenda kiwango hicho kikaongezeka sambamba na kuongeza nafasi za ajira kwa Wazanzibari watakaoajiriwa na kampuni za Huwaei na Erricson zinazofanya kazi ya kufunga mitambo hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa kitengo cha Ufundi na Mawasiliano Bwana Larry Arthur amesema mitambo hiyo ya kisasa, itamaliza tatizo la upatikanaji wa mawasiliano katika mji mkongwe wa Zanzibar pamoja na huduma ya internet katika maeneo yote ya mjini na vijijini.

Alisema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo huduma ya mawasiliano na internet itapatikana katika kiwango kinachoendana na wakati na soko la ushindani.

Kwa maelezo zaidi, tutumie ujumbe

Angalia Kama Unapata Huduma

Tafuta duka la Zantel